Dalufnin (kundinyota)

Dalufnin (Delphinus kwa Kilatini na Kiingereza) [1]. ni jina la kundinyota ndogo ya angakaskazi.

Nyota za kundinyota Dalufnin (Delphinus) katika sehemu yao ya angani
Ramani la kundinyota Dalufnin - Delphinus (kwa macho ya mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia)

Mahali pake

Dalufnin inapakana na makundinyota jirani ya Mbweha (Vulpecula), Sagita (Sagitta), Ukabu (Aquila), Dalu (Ndoo) (Aquarius), Mwanafarasi (Equuleus) na Farasi (Pegasus).

Jina

Dalufnin ilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2]

Jina la Dalufnin linatokana na Kiarabu دلفين dulfiin ambalo ni umbo la jina asilia la Kigiriki δελφίς delfis (baadaye delphinus kwa tahajia ya Kilatini[3]) ambayo ni jina kwa nyangumi mdogo mwenye meno anayeitwa pomboo kwa Kiswahili.

Wagiriki wa Kale waliwatazama akina pomboo kama wasaidizi wa mabaharia[4] na viumbe watakatifu wa miungu kama Poseidon (mungu wa bahari). Imani hii ilileta hadithi mbalimbali katika mitholojia ya Kigiriki ambako pomboo walitekeleza shughuli kwa niaba ya miungu yao. [5]

Delphinus - Dalufnin ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kwa jina la Delphinus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Del'. [6]

Nyota

Nyota za Dalufnin kwa jumla ni dhaifu; angavu zaidi ni Alfa, Beta, Gamma na Delta zinazofanya pembenne kama trapeza iliyoitwa pia „jeneza ya Ayubu“ [7]. Jina hili liliingia pia katika wimbo "Job's Coffin" wa mwimbaji Tory Amos.

Nyota za Alfa na Beta zina majina ya ajabu yaani Rotanev na Sualocin. Ukisoma majina haya kinyume unapata jina la "Nicolaus Venator" amabalo ni umbo la Kilatini la "Niccolò Cacciatore"[8] aliyekuwa msaidizi wa mwanaastronomia Mwitalia Guiseppe Piazzi[9].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
β6Rotanev3,63m80F5 IV
α9Sualocin3,77m240B9 IV
γ123,9mK1 IV + F7 V
ε2Deneb Dulfim4,03m358B6 III
δ114,43m223F1 V

Tanbihi

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Delphinus” ukurasa 321 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331