Paralaksi inasababisha nyota (njano) kuonekana mahali tofauti ikipimwa kutoka sehemu mbili tofauti za obiti ya Dunia
Parsek (en:parsec, kifupi cha parallax second, kutoka maneno paralaksi na sekunde) ni kipimo cha umbali kinachotumiwa katika astronomia kwa kutaja umbali kati ya nyota na violwa vingine vya angani. Kifupi chake ni pc.
Umbali wa parsek 1 ni sawa na miakanuru 3.26 au karibu kilomita trilioni 31 au mita 3.0857×1016.
Msingi wa kipimo hiki ni hali ya paralaksi inayosababisha ya kwamba nyota inaonekana mahali tofauti kama inaangaliwa kutoka sehemu moja kwenye obiti ya Dunia ikizunguka Jua au kutoka sehemu nyingine kinyume chake. Tofauti hii ilhali umbali wa Jua-Dunia unajulikana inaruhusu kupiga hesabu ya trigonometria na kugundua umbali wa nyota iliyopimwa.
Kwa kutaja umbali mkubwa sana kuna pia vizio vya kiloparsek (kpc), megaparsek (Mpc) na gigaparsek (Gpc).
Wanaastronomia hupendelea kutaja umbali kwa parsek kuliko miakanuru.
Parsek na Kiloparsek
Umbali kati ya nyota jirani hutajwa kwa Parsek. Kama umbali unazidi parsek 1,000 kizio cha Kiloparsek kinatumiwa, kwa mfano kutaja umbali kati ya sehemu tofauti ya galaksi moja au ndani ya kundi la galaksi.
Kitovu cha Njia Nyeupe (galaksi yetu) kina umbali wa kiloparsek 8 (miakanuru 26.000) kutoka Dunia; Njia Nyeupe huwa na kipenyo cha takriban 34 kpc (miakanuru 110.000)
Galaksi jirani ya Andromeda iko kwa umbali wa 780 kpc (miakanuru milioni 2.5) kutoka Dunia
Megaparsek na gigaparsek
Umbali wa milioni moja parsek huitwa Megaparsek (Mpc). Umbali kati ya galaksi au kati ya makundi ya galaksi hutajwa kwa megaparsek. Zaidi ya megaparsek 1,000 hutajwa kwa Gigaparsek (Gpc). Gigaparsek 1 inalingana na miakanuru bilioni 3.26
Mifano
Galaksi ya Andromeda iko takribani 0.78 Mpc (miakanuru 2.5) kutoka Dunia.
Kundi la galaksi lililo karibu (Virgo Cluster) lipo kwa umbali wa 16.5 Mpc (miakanuru 54) kutoka dunia [1]
Galaksi ya RXJ1242-11 iliyo na shimo jeusi kubwa kama Njia Nyeupe huwa na umbali wa takriban 200 Mpc (miakanuru milioni 650) kutoka Dunia
Upeo wa mwisho wa ulimwengu unaoweza kutazamiwa unakadiriwa kuwa na nusukipenyo cha 14.0 Gpc [2]